Utangulizi:
Ugonjwa wa vikope ni ugonjwa wa maambukizi kwenye macho yatokanayo na kimelea kiitwacho Clamydia Trachomatis Vimelea vya ugonjwa huu husambazwa na nzi wa majumbani kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Ni ugonjwa unaoanzia utotoni na madhara ya kupata vikope kutokea ukubwani ikiwa mtoto hata pata tiba sahihi na kuimarishwa kwa usafi wake na mazingira yanayomzunguka. Vikope ni hali ya kope katika jicho kuelekea ndani ya jicho na kuanza kukwaruza kioo cha mbele ya jicho (cornea). Hali hii husabisha jeraha kwenye kioo cha jicho na jeraha linapopona huacha kovu. Kovu la kioo cha jicho huzuia mwanga wa kutosha kuingia ndani ya jicho na hivyo kusababisha uoni hafifu au hata kufikia upofu. Ugonjwa huu hupatikana zaidi katika nchi zenye hali ya hewa ya kitropik na kwenye jamii ambazo hali ya maisha na usafi wa watu na mazingira yao ni duni. Ugonjwa wa Trachoma na mengineyo yanayosababisha makovu (cornea scar) kwenye kioo cha mbele ya jicho kama vile ugonjwa wa Usubi, Surua ya utotoni, ajali za macho na mengineyo kwa pamoja yanaingia katika orodha ya magonjwa yanayosababisha upofu unaoweza kuepukika.
Dalili:
Macho kuwa mekundu, yanayotoa machozi muda wote, yenye kuuma na kuwasha. Dalili hizi zinapatikana zaidi kwa watoto wakati vimelea vya Trachoma vinashambulia nyama laini ya ndani ya vifuniko vya macho. Hatua hii ya ugonjwa kitaalamu inaitwa Clamydia conjunctivitis. Mashambulizi haya ya mara kwa mara yasipopatiwa tiba husababisha vifuniko vya jicho kujikunja na kope kuingia ndani ya jicho (vikope). Hatua ya kupatikana vikope na madhara yake ya kusababisha makovu kwenye kioo cha mbele ya jicho huonekana zaidi kwa watu wazima.
Vigezo vya utambuzi:
Kuwepo kwa vifuniko vya macho vilivyopata madhara ya mashambulizi ya Clamydia conjunctivitis kwa watoto au watu wazima. Hali hii hupatikana zaidi katika maeneo ambayo ugonjwa huo uko kwa wingi au hata maeneo mbali na hayo kwa wale ambao walishaugua ugonjwa huu siku za nyuma.
Madhara:
Kushindwa kustahimili mwanga na maumivu ya macho kwa watoto. Kwa watu wazima madhara ni maamivu makali ya macho kwa mgojwa kila anapopepesa macho kutokana na kuchomwa na vikope pamoja na kufifia uwezo wa kuona na hata kufikia upofu kutokana na makovu kwenye kioo cha mbele ya jicho.
Kinga:
Kudumisha usafi wa mwili na mazingira ya makazi
Lengo la matibabu yatolewayo:
Tiba halaiki ambapo kwenye jamii zenye wingi wa ugonjwa huu, tiba ya kumeza dawa kwa wakazi wote kwa pamoja hupunguza wingi wa vimelea vya Clamydia Trachomatis katika jamii husika. Kwa wagonjwa waliokwisha kupata vikope, operesheni ndogo ya vifuniko vya jicho ili kusawazisha kope humwondelea mgonjwa maumuvu na kumkinga asipate upofu unaoepukika.
Matokeo ya matibabu:
Matibabu muafaka na kwa wakati huwezesha kupunguza vimelea viletavyo ugonjwa huu na kuzuia kuendelea kuwepo katika jamii. Kwa wale waliokwisha kupata vikope, matibabu ya operesheni huondoa uwezekano wa kupoteza uwezo wa kuona kutokana na madhara ya vikope.